Kwanini Njia Yetu?

Maudhui Yanayoeleweka

Labda utakuwa umeona video zetu zinatumia mbinu ya kufundishia ambayo watu wengi hawajawahi kupata, haswa kwa lugha za kibiblia. Inaitwa Maudhui Yanayoeleweka, na ni moja ya njia bora zaidi za kufundisha ulimwenguni. Sio mpya, na ni rahisi kuielewa.

Kuiweka Rahisi

Kimsingi, unapojifunza lugha, jambo muhimu zaidi ni kusikia maneno mengi kwa njia inayoeleweka. Hiyo inamaanisha kuwa maudhui yaliyowasilishwa kwako yanahitaji kuwa katika muundo ambao huwasiliana wazi kabisa kinachoendelea, iwe kwa njia ya picha au vitu au vitendo. Mtu ambaye ameitetea njia hii zaidi anaitwa Stephen Krashen. Alisema kuwa “upatikanaji wa lugha hauhitaji matumizi mengi ya sheria za sarufi, na hauhitaji mazoezi ya kuchosha.” Pia alisema kuwa njia bora za kufundisha lugha ni zile ambazo hutoa Data Inayoeleweka katika hali ya msongo mdogo wa mawazo, na hutoa ujumbe ambao wanafunzi wanataka kuusikia. Ni muhimu kutowalazimisha watu kuzungumza mapema katika kujifunza lugha ya pili, lakini waruhusu wanafunzi waanze kuzungumza wanapokuwa tayari. Wanafunzi wanaboresha uwezo wao unapowapa habari inayowasiliana na data inayoeleweka, badala ya kuwalazimisha kuzungumza na kisha kuwasahihisha. Kama utakavyoona kwenye video zetu, tunajumuisha njia hizi zote za ufundishaji, na wanafunzi ulimwenguni kote wanaona kuwa kujifunza Kiebrania hakuchanganyi na hakuogopeshi kuliko walivyodhani. Unaweza kusoma kile ambacho baadhi yao wanakisema hapa.

Sema Kwaheri kwa Msongo wa Mawazo

Kanuni nyingine muhimu ya kujifunza lugha ambayo Stephen Krashen anazungumzia ni kwamba lazima kusiwe na msongo wowote wa mawazo katika mchakato wa kujifunza. Ikiwa wanafunzi wanajisikia kutishwa au wapo katika hali ya kujihami, basi, kizuizi cha akili kinaongezeka na kinazuia kujifunza lugha kutokea. Kadiri wanafunzi wanapojisikia urahisi, kutiwa moyo, na kuamini kuwa mafanikio yanawezekana kwao, ndivyo watakavyoingiza lugha zaidi ndani. Hadi sasa, njia kuu ya mtu kujifunza Kiebrania kwa njia hii imekuwa kusoma huko Israeli kwa miezi au miaka. Lakini tunapaswa kukumbuka kuwa mshtuko wa utamaduni, chakula cha kigeni, gharama kubwa ya maisha, kuikosa familia nyumbani, kumzoea mwanachumba mwingine anayeishi naye, na kulazimika kupitia mazingira mapya ya kuongea Kiebrania cha kisasa (pamoja na Kiebrania cha Biblia darasani) hivi vyote vinaweza kuongeza msongo mkubwa wa mawazo, ambao utapelekea kuzuia mchakato wa kujifunza lugha. Wakati mwingine watafsiri wa Biblia kutoka nchi nyingine wanapambana na maisha katika Israeli, sio kwa sababu ya ubora wa programu yao au matunzo wanayopata kutoka kwa walimu, lakini ni kwa sababu tu lazima wazoee vitu vingi vipya kwa mara moja na wanazikosa familia zao.

Kwa hivyo swali letu ni kwamba, tunawezaje kuwatumikia vizuri kaka na dada zetu? Jibu ni: wape fursa ya kujifunza kutoka kwa faraja ya nyumba zao wenyewe.  Video za bure ambazo unaweza kurudisha nyuma na kurudia vile vile unavyohitaji, kwa kasi yako mwenyewe haziogopehsi, hata kidogo! Hakuna wanafunzi wengine ambao wangeweza kuyacheka makosa yako, hakuna mwalimu ambaye angeweza kukosa uvumilivu (nimekuwa mmojawapo wa kukosa uvumilivu na wanafunzi!). Hauna wasiwasi juu ya shamba lako nyumbani, wala kumkosa mwenzi wako na watoto. Na ikiwa utapata nafasi ya kusafiri kwenda Israeli, tayari utakuwa na mwanzo mzuri kwa Kiebrania ili kuutumia vizuri wakati wako huko! Mwisho wa siku, tunatumaini video zetu zitalitumikia vizuri Kanisa la ulimwengu na kusawazisha fursa zilizopo ili kila mtu apate nafasi sawa, isiyo na msongo wa mawazo ya kujifunza Kiebrania cha kibiblia. Na tunawalika wengine wanaofundisha njia hii kujiunga nasi katika kufanya rasilimali nyingine za Data Inayoeleweka zipatikane bure!

Tunapendekeza sana kutazama video tatu zifuatazo za Stephen Krashen mwenyewe akielezea sayansi na nadharia ya njia tunayotumia, na pia kanuni zaidi za kufanikiwa katika upatikanaji wa lugha. Ingawa video ni za zamani, maudhui yaliyomo bado yanafaa na yanasaidia leo kama ilivyokuwa hapo awali. Kwa wale ambao wangependelea kusikiliza sauti zilizoingizwa katika mtandao (podcast) badala ya kutazama video, unaweza kusikiliza vipindi viwili vya Andrew juu ya kujifunza lugha ambavyo vinajumuisha na sauti ya Krashen anapofundisha hapa chini na zaidi.